Barakoa za mashabiki zawa gumzo katika mechi ya Simba SC na AS Vita ya DR Congo

03 Abril, 2021

Simba imefuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa kishindo huku ikijihakikishia uongozi wa kundi A la mashindano hayo baada ya leo kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-1 mbele ya klabu ya AS Vita ya DR Congo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Mabao ya Clatous Chama aliyefunga mawili na mengine mawili yaliyopachikwa na Rallly Bwalya na Luis Miquissone yalitosha kuifanya Simba ifikishe pointi 13 ambazo hazitoweza kufikiwa na timu nyingine yoyote kwenye kundi hilo hata kama itapoteza mechi ya mwisho dhidi ya Al Ahly ya Misri ugenini

Ni mechi ambayo ilikuwa na utaratibu wa tofauti na uliozoeleka kwa mechi za soka Tanzania kwani mashabiki walikaa kwa kupishana umbali wa siti tatu na pia kuvaa barakoa ikiwa ni masharti ya kukabiliana na Covid-19.

Kabla ya mechi ya leo, Simba walicheza bila uwepo wa mashabiki katika mechi ya nyuma ya kundi hilo dhidi ya Al Merrikh uliochezwa Machi 16 ambapo waliibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Wenyeji Simba waliotawala mechi hiyo kwa kiasi kikubwa, walifunga bao la kwanza katika dakika ya 30 ya mchezo kupitia kwa Luis Miquissone aliyeunganisha kwa shuti kali pasi ya Clatous Chama.

Hata hivyo bao hilo lilidumu ndani ya muda mfupi kwani dakika ya 32, Zemanga Soze aliipa AS Vita bao la kusawazisha kwa shuti kali la mbali ambalo lilimshinda kipa Aishi Manula.

Wakati wengi wakitegemea mechi hiyo iende muda wa mapumziko huku timu hizo zikiwa sare, Simba walipata bao la pili kupitia kwa Clatous Chama ambaye aliunganisha kwa ustadi pasi ya Mohamed Hussein kutokea kushoto mwa uwanja.

https://twitter.com/SimbaSCTanzania/status/1378378328432869378

Mara baada ya mapumziko, Simba walilazimika kusubiri hadi dakika ya 66, kupata bao la tatu kupitia kwa Rally Bwalya aliyeunganisha kwa shuti kali pasi ya Chama na Chama huyohuyo alifunga bao la ushindi katika dakika ya 83 akimalizia pasi ya Shomari Kapombe.

Katika mechi nyingine ya kundi hilo, Al Merrikh ya Sudan ilitoka sare ya mabao 2-2 na Al Ahly ya Misri.

Matokeo hayo yameifanya Al Ahly ibaki nafasi ya pili ikiwa na pointi 8, AS Vita iko nafasi ya tatu ikiwa na pointi tano na Al Merrikh iko mwishoni ikiwa na pointi mbili.